Ijumaa, 5 Desemba 2014

Mwasabwite kukonga Tamasha la Krismasi

 index

Na Mwandishi Wetu MWIMBAJI wa nyimbo za injili nchini Edson Mwasabwite anayetamba kwa sasa na kibao chake kijulikanacho kwa jina la ‘Ni kwa Neema na Rehema’ amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi katika Tamasha la Krismasi litakalofanyika katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Songea Desemba mwaka huu. Mwasabwite alisema amejipanga kikamilifu kukonga nyoyo za mashabiki wake katika tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Desemba 25, 26 na 28 hivyo mashabiki zake wajitokeze kwa wingi kupata burudani ya nguvu kutoka kwake. Mwasabwite alisema mwaka huu watanzania wakae mkao wa kula kwa kusifu na kuabudu katika Tamasha la Krismasi kwani tayari amezindua albamu yake ya pili ijulikanayo kwa jina la ‘Asilimia mia Mungu amenihurumia’ yenye nyimbo tisa. “Nimejipanga vizuri kutoa burudani kwa mashabiki wangu katika tamasha la mwaka huu la Krismasi kwani maandalizi ni mazuri, safari hii itakuwa zaidi ya mwaka jana kwa sasa nina nyimbo nyingi zitakazowabariki mashabiki zangu na tayari nimeshazindua albamu mpya,” alisema Mwasabwite. Aidha amempongeza Mkurugenzi wa Msama Promotions kwa kuweza kuandaa Tamasha kubwa la Kikristo lenye mafanikio makubwa kwa kuweza kuwakutanisha waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kutangaza injili Tanzania. “Makampuni ya Msama yanaaminika na kukubalika kwa watanzania na nchi nyingine za jirani ndio maana hata tamasha linafanikiwa, tunaomba wananchi waendelee kununua kazi zetu, tunaomba sapoti kutoka kwa waumini na mashabiki wa muziki wa Injili,” alisema Mwasabwite.

 

MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA KUJITOLEA DUNIANI

Siku ya Kimataifa ya Kujitolea Duniani huadhimishwa tarehe 5 Desemba kila mwaka kwa lengo la kutambua mchango wa kujitolea unaotolewa kwa ajili ya maendeleo katika jamii tunamoishi, kitaifa na kimataifa.
Kujitolea hujumuisha hiari, umoja, utu na kuaminiana na kunatoa fursa muhimu katika kupambana na maradhi, ujinga, umasikini, hifadhi ya mazingira na maeneo mengi ya kimaendeleo ambayo yanahitaji msukumo.

Aidha, kujitolea kunatoa mchango muhimu katika kushughulikia majanga pale yanapotokea, kuimarisha umoja katika jamii na kuboresha maisha ya watu.

Tanzania kama sehemu ya jamii ya Kimataifa itaadhimisha siku hiyo katika katika ukumbi wa Chuo cha Utalii kilichopo karibu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),saa mbili na nusu asubuhi.
Kaulimbiu ya Maadhimisho hayo mwaka huu ni ‘Ushiriki na Ushirikishwaji katika kuleta maendeleo  katika ngazi zote za mitaa, taifa na kimataifa.’

Katika maadhimisho hayo, wananchi hasa vijana watashiriki katika mdahalo kuhusu umuhimu wa kujitolea kwa ajili ya kuleta maendeleo. Aidha, kutakuwa na shuhuda na maonyesho ya taasisi zinazoshiriki katika shughuli za kujitolea ili kuhamasisha na kufufua moyo wa kujitolea miongoni mwa jamii.

Watanzania hususan Vijana wanahamasishwa kuibua shughuli za kujitolea na kushiriki katika zile zilizokwisha anzishwa  ikizingatiwa kuwa wao ndiyo nguvu kazi kubwa ya jamii.

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo inawakaribisha wananchi wote kushiriki katika maadhimisho hayo muhimu ili kushiriki katika mdahalo huo na kujionea jinsi watu mbalimbali wanavyotoa mchango mkubwa katik jamii kupitia shughuli za kujitolea.
Top of Form
Bottom of Form
Bottom of Form

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni